Wakati wananchi wa Zanzibar wakiendelea kusubiri tarehe ya kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu wa marejeo, kimya kizito kimeendelea kutawala mazungumzo ya kutafuta muafaka wake.
Awamu ya nne ya mazungumzo hayo ilifanyika mjini hapa jana na kuhudhuriwa na viongozi wa kitaifa akiwamo Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad (pichani) anayedai alikuwa mshindi katika uchaguzi huo wa Oktoba 25, mwaka huu.
Viongozi hao walianza kuingia mmoja moja Ikulu Zanzibar kuanzia saa 4:00 asubuhi tayari kwa mazungumzo chini ya Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohammed Shein.
Hata hivyo, hakuna taarifa yoyote iliyotolewa baada ya kumalizika kwa mazungumzo hayo.
“Mimi siyo Msemaji wa mazungumzo hayo pamoja na kufanyika, watafuteni watu wa Ikulu wao wanaweza kuwa wanafahamu kilichoendelea,” alisema Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar, Mohamed Aboud.
Aboud ambaye pia ni Msemaji Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), alisema pamoja na bosi wake kuwa mshirika wa mazungumzo hayo, bado hafahamu kinachoendelea tangu kuanza kukutana baada ya Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (Zec), Jecha Salim Jecha, kufuta matokeo ya Uchaguzi Mkuu Oktoba 28, mwaka huu visiwani humu.
Juhudi za kumpata Katibu Mkuu Kiongozi Zanzibar, kuzungumzia suala hilo hazikufanikiwa baada ya simu yake ya kiganjani kutopokelewa mara kadhaa.
Hata hivyo, Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu, Hassan Khatib, alisema pia hafahamu kilichoendelea katika meza ya mazungumzo hayo. “Sifahamu chochote, nasikia tu kuna mazungumzo, lakini kinachoendelea sifahamu,” alisisitiza Khatib. Katibu wa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Issa Kheir, alisema: “Ni kweli Maalim Seif ameendelea na mazungumzo, lakini sifahamu kinachoendelea katika mazungumzo hayo.”
Aliongeza: “Mazungumzo haya yanahudhuriwa na Makamu wa Kwanza wa Rais, Maalim Seif Sharif Hamad, pekee siye bado hajatuambiwa chochote na hatufahamu kilichoendelea katika mazungumzo hayo.” Hata hivyo, alisema ni muhimu kuvuta subira wakati viongozi wakiendelea kutafuta ufumbuzi wa mgogoro huo.
Mkurugenzi wa Mipango na Uchaguzi wa CUF, Omar Ali Sheikh, alisema kuwa uchaguzi wa Oktoba 25 ulikuwa huru na wa haki na kumtaka Jecha kutengua uamuzi wake na kurudi kukamilisha kazi ya kuhakiki na kumtangaza mshindi katika uchaguzi huo.
“Mchezo wa kurudia uchaguzi sawa na kuchezea Katiba na sheria CUF hatutaki msamiati huo,” alisema Sheikh kabla ya mazungumzo hayo kufanyika asubuhi na kumalizika mchana. Hata hivyo, Zec imetangaza rasmi katika Gazeti la Serikali kufutwa kwa uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, mwaka huu na kuwataka wananchi kujitayarisha kwa uchaguzi wa marejeo baada ya kutagazwa tarehe ya kufanyika uchaguzi huo. Washirika wengine katika meza ya mazungumzo hayo ni Rais mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ali Hassan Mwinyi, Marais wastaafu wa Zanzibar, Dk. Salmin Amour na Amani Abeid Karume pamoja na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi.
Post a Comment