Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Magufuli, anatarajiwa kuzifuta wizara 15 kati ya zilizopo sasa na kubaki na baraza dogo litakalokuwa na wachapakazi makini ili kutimiza dhamira yake ya kubana matumizi na kuinua maisha ya Watanzania.
Kadhalika, inaelezwa kuwa Dk. Magufuli aliyeahidi kuleta mabadiliko ya kweli wakati akiomba kura kwa Watanzania kabla ya kuibuka na ushindi wa asilimia 58.46 dhidi ya wapinzani wake katika uchaguzi mkuu Oktoba 25, sasa yuko mbioni kutangaza baraza lake la mawaziri litakalokuwa na wizara 15, idadi inayofanana kwa kiasi kikubwa na ile ya Baraza la Mawaziri la miaka ya 1980 lililoundwa na Rais wa Awamu ya Kwanza, Baba wa Taifa hayati Mwalimu Julius Nyerere.
Serikali ya awamu ya nne ya Rais Jakaya Kikwete, ilimaliza muda wake Novemba 5, 2015 ikiwa na Wizara 30. Kadhalika, alipoingia kwa mara ya kwanza mwaka 2005, Rais Kikwete alikuwa na serikali kubwa yenye mawaziri na naibu wao zaidi ya 60.
Kufikia leo, Rais Magufuli aliyeapishwa Novemba 5, mwaka 2015, tayari ameshamteua Mbunge wa Ruangwa, Kassim Majaliwa, kuwa Waziri Mkuu wa serikali yake ya awamu ya tano na Ijumaa iliyopita alizindua rasmi Bunge la 11.
Chanzo kimoja cha uhakika kimedokeza jana kuwa hivi sasa, tayari Rais Magufuli kwa kushirikiana na wasaidizi wake, ameshakamilisha sehemu kubwa ya mchakato wa kuunda baraza lake la mawaziri na kwamba, kinachosubiriwa sasa ni kulitangaza wakati wowote kuanzia sasa.
Chanzo hicho kilidai kuwa Dk. Magufuli ambaye amejichimbia mjini Dodoma tangu mwishoni mwa wiki iliyopita, anatarajiwa kutangaza baraza lake dogo la mawaziri wakati wowote kuanzia leo.
“Halitakuwa sawa na hili alilomaliza nalo Rais Kikwete… na wala halitakuwa na watu wengi kama lile aliloingia nalo kwa mara ya kwanza Rais Kikwete mwaka 2005. Ni baraza dogo tu na wizara kadhaa hazitakuwapo,” kilisema chanzo hicho.
Kwa mujibu wa ibara ya 55 (1) ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, mawaziri wanakuwa wajumbe wa Baraza la Mawaziri na pia kwa mujibu wa ibara ya 54, mawaziri huteuliwa na rais baada ya kushauriana na Waziri Mkuu.
“Kuna mambo madogo bado hayajakamilika… baada ya hapo Mheshimiwa Rais atalitangaza Baraza la Mawaziri siku yoyote kuanzia leo. Kimsingi mkakati wake ni kuwa na baraza dogo lenye wizara 15,” kilieleza chanzo hicho.
Aidha, ilielezwa zaidi kuwa sura kadhaa katika baraza hilo dogo zitakuwa mpya na kwamba, mawaziri waliokuwamo katika serikali ya awamu ya nne wana nafasi ndogo ya kuteuliwa katika baraza hilo.
“Kwa kiasi fulani Baraza hili jipya linafanana na lile la Serikali ya Mwalimu Nyerere miaka ya 1980… lina wizara chache sana, zenye lengo la kubana matumizi ya serikali lakini likiwa na uhakika wa kuchapa kazi usiku na mchana ili kutimiza lengo la Rais Magufuli katika kuwaletea maisha bora Watanzania,” chanzo kiliongeza.
Kumbukumbu zinaonyesha kuwa miaka ya 1980, Mwalimu Nyerere alikuwa na serikali yenye wizara 15; ambazo ni Wizara ya Elimu; Wizara ya Mipango; Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa; Wizara ya Mambo ya Ndani; Wizara ya Ujenzi; Wizara ya Mawasiliano na Uchukuzi na Wizara ya Kazi na Ustawi wa Jamii.
Wizara nyingine wakati huo ni Wizara ya Habari na Utamaduni; Wizara ya Afya; Wizara ya Nishati, Madini na Maji; Wizara ya Sheria; Wizara ya Viwanda na Biashara; Wizara ya Kilimo na Wizara ya Fedha.
==>kandiliyetu.com
Post a Comment