Jukwaa la Katiba Tanzania (Jukata), limemshauri Rais Dk. John Magufuli, kufufua upya mchakato wa Katiba mpya.
Jukata imesema mchakato wa Katiba mpya utasaidia kuwaunganisha Watanzania baada ya kugawanyika vipande kutokana na matokeo ya uchaguzi ikiwamo kufutwa kwa Uchaguzi Mkuu Zanzibar.
Mwenyekiti wa Bodi ya Jukata, Deus Kibamba, aliyasema hayo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.
Kibamba alisema pamoja na vipaumbele vingi alivyoahidi Rais Magufuli kutekeleza, lakini mchakato wa Katiba mpya kiwe ni kipaumbele kingine muhimu cha kuwaunganisha Watanzania waliotawanyika.
“Tunaomba Rais kukamilisha mchakato wa Katiba mpya kwa kuanzia mdororo uliopo ili kusaidia kupandisha kiwango cha muafaka wa kitaifa hadi kufikia hatua za kura za maoni,” alisema.
Alisema taarifa zilizowafikia ambazo siyo rasmi zinaeleza kuwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec), baada ya kumaliza viporo vya uchaguzi katika majimbo na kata yaliyobaki, wataandaa utaratibu wa kura za maoni.
Kibamba alisema itakuwa hatari kwa nchi kuitisha kura za maoni bila kupatikana kwa muafaka kwa pande zote juu ya mchakato wa upatikanaji wa Katiba inayopendekezwa.
Alisema Katiba inayopendekezwa imewagawa watu kwenye makundi mawili ambapo wapo wanayoikubali na wengine wamekataa kuiunga mkono na kama italazimishwa, hiyo itakuwa siyo Katiba mpya.
Aliongeza kuwa baadhi ya sheria hivi sasa tayari zimepitwa na wakati hivyo itakuwa busara sheria zote zinazohitajika kwa ajili ya utekelezaji kutungwa upya. Alisema suala hilo litafanikiwa mara Rais Magufuli atakapounda baraza lake la mawaziri na kuandaa miswada kwa ajili ya marekebisho ya sheria mbili
==>IPPMEDIA
Post a Comment