Baada ya kuapishwa kushika madaraka ya Rais, kibarua kizito cha Dk John Magufuli ni kuunda Baraza la Mawaziri litakaloendana na kasi ya kaulimbiu yake ya ‘Hapa kazi tu’, ambalo ni wazi litajaa sura nyingi mpya.
Kujaa kwa sura mpya katika baraza hilo kutokana idadi ya wabunge waliokuwa mawaziri na naibu mawaziri katika Serikali iliyomaliza muda wake kupungua kutoka 55 walioanza na Rais Jakaya Kikwete katika awamu yake ya pili hadi 23, kati yao 20 wa majimbo na watatu wa viti maalumu waliofanikiwa kurudi katika Bunge la 11.
Uchambuzi uliofanywa na Mwananchi umebaini kuwa wengi wa mawaziri hao ama waliangushwa wenye majimbo yao ya uchaguzi, hawakupitishwa na CCM kuwania tena ubunge, hawakugombea tena ubunge au walifariki dunia.
Baadhi ya wabunge wateule waliokuwa mawaziri katika Serikali iliyopita huenda wakawa na nafasi ya kuteuliwa tena katika baraza jipya la mawaziri la Rais Magufuli, huku wale walioanguka wakisubiri huruma ya rais huyo kwa nafasi mbalimbali za uteuzi, zikiwamo 10 za wabunge wa kuteuliwa
Maoni ya wachambuzi
Akizungumzia Baraza la Mawaziri linalotarajiwa, mchambuzi wa masuala ya kisiasa na Mhadhiri wa Chuo Kikuu Dar es Salaam, Dk Benson Bana alisema Rais Magufuli amekuwa waziri kwa miaka takribani 20, hivyo anajua kati ya mawaziri waliopita nani mzembe na nani mchapakazi, jambo ambalo litamfanya ateue watu sahihi.
“Tatizo la nchi yetu ni mawaziri wanaoteuliwa, wengi wanajilimbikizia mali na kuwa karibu na wafanyabiashara. Wapo wabunge walikuwa mawaziri wanaoweza kwenda na kasi yake (Dk Magufuli).
“Kwanza amejipa muda wa kutosha, hakutaka kuwahi kuteua, nadhani anajipanga ili kupata watu sahihi. Watanzania watarajie mshangao katika uteuzi wake, usisahau kuwa ana nafasi 10 za kuteua wabunge ambao anaweza kuwapa uwaziri,” alisema.
Dk Bana alifafanua kwamba rais huyo ni lazima awe na mawaziri makini kwa sababu Bunge la kumi na moja litakaloanza vikao vyake Novemba 17 litakuwa na mvutano mkali, hasa kutoka wa wabunge wa vyama vya upinzani ambavyo vimetoka kujeruhiwa katika Uchaguzi Mkuu.
Hata hivyo, Dk Bana alisema Dk Magufuli kama akishindwa kujipanga kwa awamu yake ya kwanza ya miaka mitano atapata aibu kubwa, jambo alilodai kuwa ni vigumu kutokea.
“Anatakiwa kujitahidi kuwa na Baraza la Mawaziri ambalo halitakumbwa na kashfa kama ile ya Escrow au Dowans,” alisisitiza.
Kwa upande wake Profesa wa Uchumi katika Kilimo wa Chuo Kikuu cha Sokoine (SUA), Damian Gabagambi alisema tatizo la Tanzania si sera wala sheria mbovu, akifafanua kuwa hata Dk Magufuli alipokuwa Waziri wa Ujenzi aliweza kufanya mambo mazuri.
“Naona tatizo ni uzembe tu na umakini. Dk Magufuli aliwahi kusema kuwa ataingia mikataba na mawaziri wake ili kama wakishindwa kutekeleza jambo awawajibishe. Nadhani hili ni wazo zuri.
“Yule atakayeshindwa akae pembeni. Pia anatakiwa kuteua watu wasio na kashfa, nadhani uzoefu wake serikalini umempa mwanga na sasa atakuwa anawajua mawaziri wazembe na wachapakazi,” alisema.
Alifafanua kuwa baraza hilo linapaswa kuchanganywa mawaziri wapya na wa zamani wachache, ili kuondoa “kufanya kazi kwa mazoea”.
Mawaziri wa zamani
Hadi anaondoka madarakani, Rais Jakaya Kikwete katika baraza lake alikuwa na mawaziri na naibu mawaziri 55, wakiwamo 16 ambao alianza nao tangu 2005.
Kati yao, mawaziri 12 walishindwa kura ya maoni ndani ya CCM, sita waliangushwa katika Uchaguzi Mkuu, watatu walikuwa wabunge wa kuteuliwa na rais na hawakugombea, wawili walifariki dunia na sita hawakugombea ubunge.
Katika orodha hiyo, aliyekuwa Waziri wa Fedha, Saada Mkuya baada ya kuteuliwa na Rais Kikwete kuwa mbunge, amegombea ubunge katika Jimbo la Kijitoupele, Zanzibar ambalo bado halijafanya uchaguzi.
Pia mawaziri waliobahatika kurudi bungeni ni Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Sofia Simba, Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Angela Kairuki na Naibu waziri wa Katiba na sheria, Ummy Mwalimu.
Katika orodha ya mawaziri 55 yupo Dk Magufuli na Samia Suluhu Hassan waliochaguliwa kuwa Rais na Makamu wa Rais.
Katika uteuzi wake, Rais Magufuli anaweza kurejesha baadhi ya wabunge waliokuwa mawaziri, pia kuchagua wabunge nje ya hao au kuteua ambao sasa siyo wabunge, lakini vyovyoite hawatarajiwi kuwa wengi.
Pia, Dk Magufuli anaweza kutumia utaratibu uliomwibua yeye, wakati wa Rais mstaafu wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa alipoteua sura nyingi mpya za wabunge na kuwapa uwaziri.
Pia upo uwezekano wa kuteua wabunge wapya kimikoa au kikanda uliokuwa unatumiwa na mtangulizi wake ambao utakumbwa na changamoto kutokana na baadhi ya mikoa kuwa upungufu wa wabunge wa chama chake.
Mkoa wa Kilimanjaro mathalan, waliokuwa mawaziri watatu wameshindwa ubunge, akiwamo Anne Kilango (Naibu-Elimu), Aggrey Mwanri (Naibu-Tamisemi) na aliyewahi kuwa Waziri wa Viwanda, Dk Cyril Chami, huku wakibaki mawaziri wa zamani mawili.
Endapo Dk Magufuli atafuata utaratibu wa kimikoa, nyota inaweza kuwawakia tena Profesa Jumanne Maghembe (Mwanga) na aliyekuwa waziri wa Uvuvi na Mifugo, Dk David Mathayo David aliyevuliwa uwaziri katika sakata la Operesheni Tokomeza.
Wadadisi wa masuala ya kisiasa wanajiuliza endapo pia, Rais Magufuli anaweza kuwakumbuka mawaziri waliotoswa kutokana na kashfa ya Akaunti ya Tegeta Escrow, Profesa Anna Tibaijuka (Ardhi) na Profesa Sospeter Muhongo (Nishati na Madini).
Mawaziri walioshinda ubunge
Waliokuwa mawaziri ambao kwa sasa ni wabunge wateule ni; George Simbachawene (Nishati na Madini), Juma Nkamia ( Naibu-Habari), Lazaro Nyarandu (Maliasili na Utalii), Mahmoud Mgimwa (Naibu-Maliasili na Utalii), Charles Kitwanga (Naibu-Nishati na Madini).
Charles Mwijage (Naibu-Nishati na Madini), Stephen Masele (Naibu-Muungano), William Lukuvi (Ardhi), Mwigulu Nchemba (Naibu-Fedha), Jenista Mhagama (Sera, Uratibu Bunge), Gerson Lwenge (Naibu-Maji).
Wengine ni Dk Harrison Mwakyembe (Afrika Mashariki), January Makamba (Naibu-Mawasiliano), George Mkuchika (Utawala Bora), Profesa Jumanne Maghembe (Maji), Dk Shukuru Kawamba (Elimu), Hawa Ghasia (Tamisemi), Dk Mary Nagu (Mahusiano na Uratibu), Dk Charles Tizeba (Naibu-Uchukuzi) na Dk Hussein Mwinyi (Ulinzi)na Janet Mbene (Naibu-Viwanda na Biashara).
Walioanguka kura ya maoni
Waliokuwa mawaziri ambao waliangushwa kura ya maoni Dk Binilith Mahenge (Mazingira), Adam Malima (Naibu-Fedha), Dk Seif Rashid (Afya), Dk Pindi Chana (Naibu-Wanawake, Jinsia na Watoto), Dk Titus Kamani (Uvuvi), Kaika Telele Naibu-Uvuvi) na Amos Makala (Naibu-Maji).
Dk Abdulla Juma Abdulla (Naibu-Afrika Mashariki), Mathias Chikawe (Mambo ya Ndani), Mahadhi Juma Maalim (Naibu-Mambo ya Nje), Pereira Ame Silima (Naibu-Mambo ya Ndani), Christopher Chiza (Uwekezaji na Uwezeshaji) na Gaudencia Kabaka (Kazi na Ajira).
Viti maalumu
Mawaziri waliokuwa wabunge wa viti maalumu ambao wamerudi mjengoni, Sofia Simba (Wanawake, Jinsia na watoto), Angela Kairuki (Naibu-Ardhi) na Ummy Mwalimu (Naibu-Katiba na Sheria).
Waliangushwa katika uchaguzi
Mawaziri walioangushwa katika uchaguzi ni Dk Stephen Kebwe (Naibu-Afya), Anne Kilango- Malecela (Naibu-Elimu), Dk Fenella Mukangara (Habari), Aggrey Mwanry (Naibu-Tamisemi), Stephen Wasira (Kilimo), Godfrey Zambi (Naibu-Kilimo).
Hawakugombea tena
Mawaziri ambao hawakugombea kabisa ubunge ni Samuel Sitta (Uchukuzi), Profesa Mark Mwandosya (Ofisi ya Rais-Kazi Maalumu) Bernard Membe (Mambo ya Nje), aliyekuwa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda na Dk Makongoro Mahanga aliyehama CCM na kujiunga na Chadema.
Pia wapo waliokuwa mawaziri baada ya kuteuliwa na Rais Kikwete kuwa wabunge lakini hawakujitosa kuwania ubunge majimboni ambao ni, Dk Asha-Rose Migiro (Katiba na Sheria), Profesa Makame Mbarawa (Mawasiliano).
Waliofariki dunia
Mawaziri wa Serikali iliyomaliza muda waliofariki dunia ni aliyekuwa Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk Abdallah Kigoda na aliyekuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Utumishi), Celina Kombani.
Post a Comment