Chama cha Mapinduzi (CCM) mkoa wa Dodoma kimesema kuwa kimejipanga kuhakikisha wananchi ambao sio wakazi wa maeneo husika mkoani humo hawashiriki kuwachagua viongozi wasiowahusu.
Katibu Msaidizi wa CCM Mkoa wa Dodoma, Othman Dunga aliyasema hayo hivi karibuni alipoongea na waandishi wa habari mkoani humo, ambapo alieleza kuwa wanafunzi wa vyuo vikuu mbalimbali waliojiandikisha katika mkoa huo lakini hawaishi maeneo hayo hawataruhusiwa kupiga kura kuwachagua wabunge na madiwani.
“Zipo taarifa kwenye mitandao ya kijamii kwamba Ukawa wameanzisha utaratibu wa kukodi magari kwa ajili ya kuwaleta wanafunzi ambao wamejiandisha hapa kwa ajili ya kupiga kura. Huu ni ushahidi tosha kwamba sio wakazi wa Dodoma,” alisema Dunga.
“CCM tumejipanga kuhakikisha hawapigi kura za kiongozi asiyewahusu, mawakala wetu watakabidhiwa orodha ya wakazi na wataisimamia hiyo,” Dunga ananukuliwa.
Kulikuwepo na taarifa zisizo rasmi kuwa kuna ‘wasamalia wema’ ambao wamejitolea kuhakikisha wanafunzi wa vyuo vikuu waliojiandikisha katika daftari la wapiga kura wakati wakiwa vyuoni na sasa wako majumbani, wanarudi katika maeneo waliyoandikishwa ili wapige kura. Kwa mujibu wa Dunga, huenda wanafunzi hao wakaambulia kupiga kura kumchagua rais pekee katika eneo walilojiandikishia walipokuwa wanasoma vyuoni hapo.
Post a Comment