Baada ya Rais Dk. John Magufuli, kuvunja ukimya kwa kumteua Kassim Majaliwa, kuwa Waziri Mkuu wa Serikali ya awamu ya tano jana, hatimaye imefahamika ni kwa nini mbunge huyo wa Ruangwa mkoani Lindi alikuwa na kila sababu ya kupata nafasi hiyo.
Majaliwa aliyekuwa hatajwi sana katika orodha ya watu waliobashiriwa kushika nafasi hiyo, alishangaza wengi baada ya jina lake kutajwa na Spika wa Bunge, Job Ndugai na kuibua shangwe kubwa.
Uchunguzi uliofanywa na Nipashe ukiwahusisha pia baadhi ya watu walio karibu na Majaliwa umebaini kuwa naibu waziri huyo wa zamani wa Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) ameipata nafasi hiyo siyo kwa bahati kama ambavyo baadhi ya watu wanaweza kudhania, bali ni kutokana na msururu wa sifa zinazokidhi aina ya Waziri Mkuu anayeendana na Rais Magufuli.
Awali, Novemba 2 mwaka huu ikiwa ni muda mfupi tu baada ya Dk. Magufuli kutangazwa kuwa mshindi wa nafasi ya urais kufuatia asilimia 58.46 ya kura halali alizopata dhidi ya wapinzani wake akiwamo Edward Lowassa aliyewakilisha muungano wa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), Nipashe ilitaja sifa kadhaa za Waziri Mkuu wa serikali ya awamu ya tano na kwa namna ya kipekee, zote sifa hizo zilizotolewa na wachambuzi wazoefu wa masuala ya siasa nchini, zinaendana moja kwa moja na Majaliwa.
“Ana sifa karibu zote zinazomfaa kuwa Waziri Mkuu wa Magufuli… hiki ndiyo kigezo kikubwa kilichombeba hadi akateuliwa kushika nafasi hiyo,” mmoja wa wachambuzi hao aliiambia Nipashe jana.
Baadhi ya wachambuzi wa masuala ya kisiasa wanahusisha pia uteuzi wa Majaliwa na dhamira ya Rais Magufuli katika utekelezaji wa ahadi zake alizotoa wakati wa kampeni za kuwania urais wakati wa uchaguzi mkuu.
Inakumbukwa kuwa maeneo 10 ambayo Magufuli alitangaza wazi kuwa amepania kuyashughulikia aingiapo madarakani ni pamoja kubana matumizi ya serikali, kuongeza mapato ya serikali kuboresha mfumo wa utendaji na ufanisi na kupitia kodi na ushuru unaowaumiza wakulima, wafugaji na wavuvi.
Pia kupitia upya baadhi ya sheria, kuorodhesha kero za wananchi, kuunda serikali ndogo, kumaliza kero za watumishi wa umma, utekelezaji wa ilani ya CCM na kupendekeza muundo wa kitaasisi ili kutekeleza ahadi yake ya kutoa Sh. milioni 50 kwa kila kijiji.
UADILIFU
Ili Dk. Magufuli atimize ahadi zake na hasa ile ya kupambana na ufisadi na rushwa, ilikuwa ni lazima awe na Waziri Mkuu asiyekuwa na chembe ya kashfa, hasa zinazohusiana na rushwa.
Katika miaka ya hivi karibuni, ikiwamo ya awamu ya nne ya uongozi wa nchi hii, kuliibuka kashfa kadhaa za ufisadi na rushwa kiasi cha kuitikisa serikali ya Rais Jakaya Kikwete mara kadhaa kutokana na vitendo vya aina hiyo.
Kashfa hizo ni pamoja na ile ya uchotwaji fedha katika akaunti ya Benki Kuu ya Malipo ya Madeni ya Nje (EPA), ukodishwaji wa mitambo ya umeme ya kampuni ya kufua umeme ya Richmond, ripoti chafu ya Msimamizi na Mkaguzi wa Fedha za Serikali (CAG) na ile ya ufisadi wa fedha za akaunti ya Tegeta Escrow kwenye Benki Kuu (BoT).
Lowassa aliwajibika kufuatia kashfa ya Richmond mwaka 2008 wakati Pinda alinusurika kwenye kashfa ya Escrow baada ya kusafishwa na Bunge. Hali hiyo inatajwa kuwa ni sababu mojawapo kubwa iliyomfikisha Majaliwa alipo sasa kwani inaelezwa kuwa kama alivyo Rais Magufuli, naye hana doa lolote kubwa linalohusisna na rushwa na ufisadi.
UKANDA
Kwa kuwa Dk. Magufuli anatokea katika mkoa wa Geita, ambao uko Kanda ya Ziwa,4 ilibashiriwa wazi kuwa Waziri Mkuu wa Serikali ya awamu ya tano atakuwa na uwezekano mdogo wa kuteuliwa kutoka katika kanda hiyo au zile za jirani.
Pamoja na ukweli kuwa, Tanzania ni miongoni mwa nchi chache duniani ambazo zimefanikiwa kupiga vita ukabila, lakini bado suala hilo limekuwa likichukuliwa kwa tahadhari kubwa.
Wafuatiliaji wa masual ya siasa nchini, wanaamini kwa vyovyote vile, Rais Magufuli atakuwa ameangalia jiografia ya nchi na kuhakikisha kuwa msaidizi wake mkuu wa shuguhuli za serikali anatoka sehemu nyingine ya nchi na siyo kwenye ukanda wao wala jirani na huko. Majaliwa anatokea mkoa wa Lindi ambao uko katika Kanda ya Kusini.
“Hii ni sababu isiyojadiliwa sana, lakini ni muhimu na kwa namna yoyote ile Rais aliizingatia katika uteuzi wake,” mchambuzi mmoja aliiambia Nipashe jana.
KUJIAMINI, MTU WA MAAMUZI MAGUMU
Mtu aliyetarajiwa kuwa Waziri Mkuu katika serikali ya Rais Dk. Magufuli alitakiwa kuwa na sifa ya kujiamini na uwezo mkubwa wa kutoa maamuzi magumu pale inapobidi.
Kutokana na unyeti wa kazi yenyewe na changamoto zinazokabili taifa kwa sasa, mtu wa sifa hii alikuwa na nafasi kubwa ya kuteuliwa na Magufuli kwani ndiyo pekee inayompa uhakika kuwa ni mtu asiyeyumba. Watu wanaomfahamu Majaliwa kwa karibu wanamuelezea kuwa yuko vizuri katika eneo hili na hivyo, kwa vyovyote vile, sifa hii pia imembeba kwa kiasi kikubwa.
Inaelezwa vilevile kuwa sifa nyingine ya Majaliwa ni uwezo mkubwa alio nao pia katika kujibu maswlai kwa ufasaha, tena bila kutanguliza ‘blaa blaa’ za kisiasa kwa masuala ya msingi. Hili alishalionyesha wakati wa kujibu maswali yaliyoelekezwa kwenye wizara yake bungeni na sasa natarajiwa pia kulionyesha zaidi wakati wa kipindi cha maswali ya papo kwa papo kwa Waziri Mkuu na pia wakati serikali itakapokuwa na hoja za kujibu, hasa kutoka kambi ya upinzani yenye wabunge 121.
ASIYEMZIDI RAIS MAGUFULI KWA UMAARUFU
Hii inatajwa kuwa ni sifa mojawapo kubwa na muhimu iliyombeba Majaliwa. Inalaezwa kuwa mara zote, uzoefu unaonyesha kuwa watu wengi waliowahi kushika wadhifa wa Waziri Mkuu ni wale wanaosifika kwa utekelezaji zaidi na siyo wenye kusaka umaarufu. Watu hawa hutakiwa kutekeleza wajibu wao kwa weledi na umakini mkubwa, lakini bila ya kumzidi Rais aliyeko madarakani kwa sifa au umaarufu huo.
Rekodi za nyuma zinaonyesha kwa mfano, nyota ya siasa ya Mwalimu Nyerere ilikuwa juu kisiasa licha ya kufanya kazi na mawaziri wakuu tofauti waliokuwa wachapakazi kwelikweli kama Rashid Mfaume Kawawa, Edward Moringe Sokoine, Cleopa Msuya na Salim Ahmed Salim.
Hata Joseph Warioba na John Malecela waliposhika wadhifa huo kwenye awamu ya pili chini ya Rais Mwinyi au Frederick Sumaye alipofanya kazi kwa miaka 10 na Rais mstaafu wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa, bado nyota za marais wao zilikuwa juu.
“Magufuli alipaswa kuwa na Waziri Mkuu asiye na nyota kali ya umaarufu kuliko yeye ili kuhakikisha kuwa malengo ya serikali yake yanatimia na siyo msaidizi wake kutumia nafasi hiyo katika kujijenga kisiasa,” mchambuzi mwingine wa siasa aliiambia Nipashe.
UWEZO KUSIMAMIA UTEKELEZAJI
Sifa mojawapo ya Waziri Mkuu mpya chini ya Dk. Magufuli ilitarajiwa kuwa ni uwezo wa kusimamia na utelekezaji wa dhati wa mipango ya serikali.
Kwa mujibu wa Dk. Magufuli, yeye hana nafasi na mawaziri wanaoendekeza kauli za ‘mchakato’, ‘tuko mbioni’ wala ‘tuko katika hatua nzuri’, bali anachotaka ni vitendo zaidi katika utekelezaji. Na mwenyewe Magufuli amedhihirisha hilo katika utendaji wake kwenye wizara mbalimbali alizowahi kuongoza, ikiwamo aliyomaliza nayo ya Ujenzi.
Dk. Magufuli alijizolea sifa kubwa kutokana na utendaji wake, hasa katika kusimamia ujenzi wa barabara sehemu mbalimbali nchini na bila kusahau alipokuwa Wizara ya Ardhi na ile ya Mifugo na Uvuvi.
Waziri Mkuu Majaliwa anatajwa kuwa ni mmoja wa wachapakazi makini na ambaye, wengi wanamtarajia ataendeleza moto wake wa kazi aliouonyesha katika kusimamia elimu akiwa Tamisemi na kumfikia Rais Magufuli au kumzidi kama mwenyewe alivyoahidi sifa za mawaziri wake zitakavyokuwa wakati wa kampeni za uchaguzi. Magufuli anatarajiwa pia kufanya vizuri zaidi kwani Tamisemi bado iko chini ya ofisi yake.
KINARA WA KWELI SHUGHULI ZA SERIKALI BUNGENI
Tangu kuanza kwa mfumo wa vyama vingi nchini Tanzania, miongoni mwa viongozi wanaokumbana na changamoto kali za wapinzani bungeni ni mawaziri wakuu.
Hawa ndiyo wamekuwa na kibarua cha kuwa vinara katika kukabili shinikizo kutoka kwa wapinzani, hasa katika kufafanua masuala ya utendaji. Majaliwa anaelezewa na wabunge wengi kuwa yuko vizuri katika eneo hili.
KUKUBALIKA NDANI, NJE CCM
Dk . Magufuli wakati akiteua Waziri Mkuu mpya, alitarajiwa kumtaja mtu mwenye sifa hii ya kukubalika na kuheshimika ndani na nje ya CCM. Wachambuzi wa masuala ya siasa wanasema Majaliwa anayo sifa hii na ushindi wake wa kishindo bungeni baada ya jina lake kuwasilishwa ni ishara kwamba kweli anakubalika, wakiamini kuwa atatekeleza kwa dhati ahadi zake na pia kulinda maslahi ya chama chake pindi atakapotakiwa kufanya hivyo.
MTU ASIYEWAZIA URAIS
Pamoja na dhamira njema ya Rais Kikwete ya kuwatumikia vizuri Watanzania, lakini moja ya matatizo yaliyomkabili ilikuwa ni kitendo cha baadhi ya mawaziri kuunda mitandao ya maandalizi ya urais kwa ajili ya uchaguzi mkuu uliopita wa 2015.
Mara baada ya kuingia madarakani mwaka 2005, baadhi ya watendaji wa serikali na wale wa CCM walianza kazi ya kuandaa mikakati na kutengeneza mitandao ya kumrithi Rais Kikwete.
Mitandao hiyo ilisababisha kuporomoka kwa utendaji wa baadhi ya mawaziri na mbaya zaidi, kulitokea kutoelewana na hata kuwapo kwa migawanyiko ya wazi.
Inaelezwa kuwa kufuatia hali hiyo, kulizuka mtindo wa baadhi ya mawaziri kubaki na kazi moja ya kuchafua wenzao huku wengine wakihangaika kujijenga kisiasa badala ya kufanya kazi waliyotumwa na rais na matokeo yake kushuka kwa utendaji katika baadhi ya wizara.
Hali hiyo ilisababisha Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuwaomba Rais mstaafu Ali Hassan Mwinyi, aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wa chama hicho, Pius Msekwa na Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, kufanya kazi ya kusuluhisha makundi ndani ya chama hicho. Ni wakati huo pia ndipo mawaziri kadhaa walitajwa wazi na Kinana kuwa ni ‘mizigo’ kwani utendajni wao ulikuwa ukilalamikiwa na wananchi karibu katika kila kona na kudhoofisha chama chao.
Majaliwa hatajwi kuwa mmoja wa watu wanaojikweza na kujipatia umaarufu kwa nia ya kutaka kuwania urais siku moja. Hii ni sababu nyingine inayotajwa kuwa imembeba hadi kuwa mrithi wa Mizengo Pinda kwa nafasi ya uwaziri mkuu.
UZOEFU SERIKALINI
Wasifu wa Majaliwa unahusisha utumishi wa miaka kadhaa katika ofisi mbalimbali za serikali, akiwahi kuwa mwalimu, mkuu wa wilaya, ubunge hadi kuwa naibu waziri wa Tamisemi. Waziri Mkuu kwa kawaida ndiye mtendaji mkuu wa serikali. Na ndiyo maana ni muhimu akawa na uelewa mpana wa namna serikali inavyofanya kazi na mifumo yake.
Mathalani, Waziri Mkuu anayemaliza muda wake, Mizengo Pinda, kabla ya kushika wadhifa huo, alikuwa na uzoefu mkubwa wa utumishi serikalini kwa kufanya kazi kwenye Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Ikulu na kuwa Naibu Waziri na waziri kamili wa masuala ya Tamisemi.
Pia mawaziri wakuu waliomtangulia waliwahi kushika nyadhifa mbalimbali serikalini kabla ya kupata nafasi hiyo. Na ndiyo maana Majaliwa amepata nafasi hii kwani uzoefu wake siyo haba, ijapokuwa hakuwahi kushika nafasi ya uwaziri kamili.
MAWAZIRI WAKUU WALIOTANGULIA
Kabla ya Majaliwa aliyeidhinishwa kwa kishindo bungeni jana, wengine waliowahi kuwa mawaziri wakuu ni pamoja na Julius Nyerere (1961-1962), Rashid Kawawa (1962 na 1972-1977) Edward Sokoine (1977-1980, 1983-1984), Cleopa Msuya (1980-1983, 1994-1995), Salim Ahmed Salim (1984-1985), Joseph Sinde Warioba (1985-1990), John Malecela (1990-1994), Frederick Sumaye (1995-2005), Edward Lowassa (2005-2008) na Mizengo Pinda (2008-2015).
==>IPPMEDIA
Post a Comment