Social Icons

Loading...

WAZEE WA KIMILA WATISHIA WALIOOKOLEWA,WAHITAJI WAFANYIWE MATAMBIKO ILI KUONDOA MIKOSI...SOMA MKASA MZIMA HAPA..


 Wazee wa kimila wa makabila ya Wakurya na Waluo wamesema watu watano waliookolewa kutoka kwenye machimbo ya Nyangalata, Kahama ambao waliwekewa matanga kabla ya kuibuka wanatakiwa kufanyiwa mambo ya kimila, vinginevyo watakufa kiajabu.

Mmoja wa wazee hao, Ghati Ryoba (61) wa Mtaa wa Mwangaza, Nyamisangura – Tarime alisema: “Mtu akidaiwa kuwa amekufa lakini baadaye akaonekana, wazee wa ukoo au wa mila humfanyia matambiko kama njia ya kuondoa mikosi kwake na kwa familia yake. Wanachukua kondoo mweusi wanamchinja kisha wanamtambikia (bharamsendola).

“Kisha wanachukua kinyesi cha kondoo (ubhuhu ghwaling’ondi) na mti mmoja unaitwa (richirya) kisha kile kinyesi kinarushwarushwa ndani ya nyumba yake na mji mzima kama kuna nyumba nyingine halafu wanachukua kile kinyesi cha kondoo na kumpaka kwenye mikono na anashikana mikono na watu.”

Mzee huyo wa kimila aliongeza kusema kuwa baada ya hapo atanawa mikono kabla ya kuruhusiwa kula na kujumuika na watu.

Alisema baada ya hapo atanyolewa kisha atakwenda kuoga “... Wengine hupeleka nywele kuzizindika kwenye mlima ambako watu hawalimi.”

Kuhusu Waluo, mzee Peter Odello wa Kitembe, Rorya alisema: “Kama inatokea mtu anadaiwa kufa na watu wakafanya matanga lakini baadaye akaonekana, lazima arudi kijijini wamfanyie matambiko.”

Alisema akirudi, wazee watachinja ng’ombe na watu watakaa tena kama walivyokaa kwenye matanga kwa siku mbili au tatu watu wakila kisha kupewa dawa inayoitwa manyasi.

Wapata misaada

Wakati wazee wakizungumzia matambiko, waathirika hao wameanza kupatiwa misaada mbalimbali ikiwamo vyakula vya lishe na nguo.

Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Halmashauri ya Mji; Joseph Ngowi alisema misaada hiyo mbali ya vyakula na nguo pia vimo vinywaji baridi.

Ngowi alisema juzi na jana, taasisi mbalimbali, watu binafsi na mashirika ya dini walijitokeza kutoa misaada hiyo .

Mmoja wa waathirika hao, Joseph Bulule ambaye hali yake imeanza kuimarika alisema msaada huo ni muhimu kwao na umewapa faraja kujua kwamba Watanzania wenzao wanawathamini.

Bulule pia aliishukuru Serikali wakiwamo watumishi wote wa idara ya afya halmashauri zote za Wilaya ya Kahama kwa jinsi walivyowahudumia tangu walipolazwa. Muuguzi katika wodi namba 2 ya hospitali hiyo, Catherine John alisema misaada kwa waathirika imetolewa kwa wakati kwa kuwa watu hao wanahitaji chakula zaidi kwa ajili ya kuboresha afya zao.

Wachimbaji hao walifukiwa na vifusi Oktoba 5, katika machimbo ya Nyangalata na baadaye kuokolewa wakiwa hai Novemba 15 baada ya kuishi shimoni kwa siku 41 wakila magome ya miti, mende na vyura.
==>Mwananchi

author

This post was written by: Author Name

Your description comes here!

Get Free Email Updates to your Inbox!

Post a Comment

CodeNirvana
© Copyright MAWINGUBONGO
Back To Top