Kigali, Rwanda. Wakati Wanyarwanda wakipiga kura ya mabadiliko ya katiba kesho ili kumuwezesha Rais Paul Kagame kuongoza muhula mwingine ,utafiti wa Ipsos unaonyesha kuwa zaidi ya asilimia 90 ya wananchi wa taifa hilo wanataka kuendelea kuongozwa na kiongozi huyo.
Akiwasilisha ripoti hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Ipsos, Virginia Nkwanzi Isingoma alisema Wanyarwanda wameonyesha kuwa na imani kubwa kwa Rais Kagame huku wakimtaka aendelee kuongoza kwa muhula mwingine.
Miongoni mwa mambo ambayo yametajwa na Wanyarwanda wengi waliohojiwa katika utafiti huo ni namna kiongozi huyo alivyoweza kurejesha amani, mshikamano na maendeleo katika taifa hilo lililopitia machafuko.
“Asilimia 92 ya watu walioshiriki wenye utafiti huu walimuelezea Kagame kama kiongozi bora mwenye haiba ya aina yake na bado wanaendelea kumuhitaji awaongoze.
Zipo sababu nyingi zilizotajwa lakini kubwa ni namna alivyoweza kusimamia amani na mshikamano wa taifa sambamba na misingi ya demokrasia ” alisema.
Matokeo hayo ya utafiti yamekuja muda mfupi kabla ya upigaji kura ya maamuzi kuhusiana na mabadiliko ya katiba ambao unatarajiwa kufanyika leo.
Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Rwanda Profesa Kalisa Mbanda amesema watu 6.4 milioni wamejiandikisha kushiriki kwenye zoezi hilo na maandalizi yote yalikwishakamilika.
“Tunatarajia upigaji kura uanze saa moja asubuhi na utakamilika saa tisa alasiri kwa mpangilio huo tunaweza kutangaza matokeo ya awali saa 11 jioni”
Post a Comment