Tangu kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani Oktoba 25, mwaka jana, aliyekuwa mgombea urais kupitia Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Edward Lowassa, jana alikutana kwa mara ya kwanza ‘uso kwa uso’ na kiongozi wa juu wa serikali ya Rais Dk. John Magufuli.
Lowassa akiwa katika ibada maalum ya kumwingiza kazini, Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Askofu Dk. Fedrick Shoo, alikutana na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa na kusalimiana.
Taarifa zinaeleza kuwa tokea kampeni za uchaguzi mkuu zilipoanza Agosti 22, mwaka jana, hadi jana kiongozi huyo aliyekuwa anaungwa mkono na vyama wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) katika kugombea urais, hakuwahi kukutana wala kusalimia na kiongozi yeyote wa juu serikali serikalini.
Majaliwa alikuwa mjini Moshi ambapo alikuwa mgeni rasmi katika ibada maalumu ya kumwingiza kazini, Askofu Dk. Shoo, ambaye ataiongoza KKKT kwa kipindi cha miaka minne ijayo.
Askofu Dk. Shoo anakuwa Mkuu wa KKKT, kuchukua nafasi ya Askofi Dk. Alex Malasusa ambaye aliliongoza kanisa hilo kwa miaka minane. Malasusa ambaye ni Askofu wa Dayosisi ya Mashariki na Pwani, alikuwa katika nafasi hiyo kwa vipindi viwili vya miaka minne kila kimoja.
Katika uchaguzi mkuu uliopita, Rais Dk. Magufuli aliibuka mshindi baada ya kupata asilimia 58.46 huku Lowassa akipata asilimia 39.97 ya kura zote halali zilizopigwa.
Hata hivyo, Lowassa alipinga matokeo hayo akidai kuwa alinyang’anywa ushindi wake na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC). Alidai kuwa takwimu zake zinaonyesha alipata zaidi ya asilimia 60 ya kura zote halali zilizopigwa.
CHANZO: NIPASHE
Post a Comment