Social Icons

Loading...

RAIS JPM USO KWA USO NA WAUZA UNGA,VITA YAANZA RASMI...SOMA HABARI KAMILI HAPA...

Mkakati wa Rais, John Magufuli, kupambana na dawa za kulevya, umeanza kuonekana baada ya Waziri wake wa Mambo ya Ndani, Charles Kitwanga, kuagiza yafanyike mabadiliko makubwa katika vitengo mbalimbali vya Idara ya Uhamiaji.
 
Moja ya idara ambazo maofisa wake watakumbwa katika mabadiliko hayo ambazo zilikuwa uchochoro wa kupitisha dawa za kulevya kwa muda mrefu, wahamiaji haramu na wanyama hai, ni viwanja vya ndege vya Kimataifa vya Julius Nyerere Dar es Salaam, Kilimanjaro (KIA) na wale waliopo katika mpaka wa Tunduma, Mtukula, Halolili na Kasumulo.
 
Mbali na maofisa hao, pia Kitwanga ameagiza kuhamishwa kwa wakuu wa upelelezi wote wa wilaya za Dar es Salaam na maofisa wa uhamiaji waliokaa kwenye kituo kimoja kwa zaidi ya miaka mitatu, huku akisema huo ni mwanzo wa mabadiliko makubwa kwenye idara hiyo.
 
Taarifa iliyotolewa jana na Wizara ya Mambo ya Ndani baada ya kikao cha Kitwanga na viongozi wa Idara ya Uhamiaji, ilimnukuu waziri huyo akiwaasa watumishi wa uhamiaji kuwa: “Watumishi wote wa Idara ya Uhamiaji wafanye kazi zao kwa kuzingatia sheria, kanuni na maadili ya kazi na waepuke vitendo vya kupokea rushwa na kusaidia wahamiaji haramu na wauza dawa za kulevya.”
 
Hatua hiyo imekuja mwezi mmoja baada ya Rais Magufuli kumsimamisha kazi, Kamishna Mkuu wa Uhamiaji nchini, Sylvester Ambokile, ili kupisha uchunguzi katika idara hiyo.
 
Taarifa iliyotolewa na Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Ikulu, Gerson Msigwa, Januari 20, mwaka huu ilisema Ambokile amesimamishwa kazi kutokana na tuhuma za rushwa, ukusanyaji mbaya wa maduhuli ya serikali, ukiukwaji wa taratibu za manunuzi na utendaji mbovu.
 
Kamishna wa Uhamiaji anayeshughulikia Utawala na Fedha, Piniel Mgonja, naye alisimamishwa kazi.
 
MATUKIO YA DAWA ZA KULEVYA
Mbali na aina mbalimbali za dawa za kulevya ambazo zimekuwa zikikamatwa ndani ya nchi na zile zinazokamatiwa nje zikiwa zimetoka Tanzania, baadhi ya matukio makubwa yaliyowahi kutikisa ni lile la Julai 2012, wakati Mamlaka ya Mapato ya Afrika Kusini (SARS), ilipokamata kilo 350 za dawa za kulevya aina ya Mandrax  zilizokuwa zikitoka Tanzania kupitia Botswana kabla ya kufika kwenye nchi hiyo.
 
Julai 2013, Watanzania wawili, Agnes Masogange na Melissa Edward, walikamatwa kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Oliver Tabwe nchini Afrika Kusini na mabegi sita yaliyodaiwa kubeba dawa za kulevya aina ya Methamphetamine maarufu kama Tik yenye thamani ya Sh bilioni 7.
 
Mamlaka za nchi hiyo zilisema hicho ni kiasi kikubwa cha dawa za kulevya kuwahi kukamatwa nchini humo.
 
Pia inaelezwa kuwa, zaidi ya Watanzania 200 wameshikiliwa kwenye magereza ya Hong Hong na China kwa tuhuma za kusafirisha dawa za kulevya.
 
Wengi wa watu hawa husafiri kwa kutumia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere na wachache wakitumia mipaka mingine.
 
WANYAMA HAI
Wakati uwanja wa Dar es Salaam ukiwa na sifa ya kusafirisha wahamiaji haramu, ule wa Kilimanjaro uliweka historia ya aina yake Novemba 24, 2010, baada ya kusafirisha wanyama hai 116 wa aina 14 wakiwamo twiga wanne.
 
Wanyama hao wanaokadiriwa kuwa na thamani ya Sh. 163,732,500, walisafirishwa kwa kutumia ndege ya kijeshi ya Qatar. 
WAHAMIAJI HARAMU
Wakati hali ikiwa hivyo kwenye viwanja vya ndege, katika mipaka mingine pamoja na kasoro nyingine, kushindwa kuthibiti wahamiaji haramu ni kati ya kashfa zinazoikumba idara hiyo.
 
Novemba 2015, polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam ilikamata wahamiaji haramu 105 raia wa Ethiopia na walidaiwa walikuwa wakipita Tanzania kuelekea nchi nyingine.
 
Machi 2015, polisi mkoa wa Dodoma walikamata wahamiaji 64  raia wa Ethiopia, ambao walikuwa wakisafirishwa kwa lori.
 
Mbali na matukio ya kukamatwa kwa wahamiaji hao ambayo yamekuwa yakijirudia kila mara, lililosikitisha ni lile la Juni, 2012, ambapo miili 43 ya raia wa Ethiopia ilikutwa kichakani katika kijiji cha Chitego, wilayani Kongwa, Dodoma.
 
Katika tukio hilo pia wahamiaji wengine 84 walikamatwa afya zao zikiwa zimedhoofu sana.
 
Watu hao walidaiwa kuwa kwenye hali hiyo kutokana na kusafirishwa kwa lori lililofunikwa hali iliyofanya wakose hewa.
 
WAZIRI KITWANGA
Taarifa iliyotolewa na wizara jana, ilimnukuu Kitwanga akisema: “Katika kuisafisha idara hiyo, uangalifu utachukuliwa ili kuhakikisha hakuna mtumishi atakayeonewa wala kupendelewa, lengo kubwa likiwa ni kuvunja mtandao wa wapokea rushwa na wale wasiowajibika.”
 
Ilisema hatua hiyo imechukuliwa baada ya utafiti uliofanywa na kuonyesha matatizo ya rushwa katika Idara ya Uhamiaji yanashika nafasi ya kwanza kwa kuwa na asilimia 30.
 
Alisema utafiti huo ulionyesha asilimia 20 inashikwa na  uongozi mbovu na asilimia 20 nyingine ni matumizi mabaya ya madaraka.
“Asilimia 15 inahusisha vitendea kazi na mifumo hafifu ya kufanya kazi, asilimia 10 huduma mbovu na asilimia tano ukabila na upendeleo,” ilisema.
 
Kikao hicho pia kilihudhuriwa na viongozi wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, wakiwemo wakuu wa idara na vitengo vya wizara hiyo.  
 
“Katika kikao hicho, Kitwanga ameagiza watumishi wote wa Idara ya Uhamiaji walioko Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Dar es Salaam na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro, wahamishwe na kupelekwa maeneo mengine nchini, wakiwamo wale wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano,” ilisema taarifa.
 
Ilisema wengine watakaohamishwa ni kutoka kitengo cha hati za kusafiria, uhasibu, hati za ukaazi na kitengo cha upelelezi, vyote vya Makao Makuu ya Uhamiaji, jijini Dar es Salaam.
 
Waziri Kitwanga pia ameagiza wakuu wote wa vitengo vya upelelezi vya wilaya za Dar es Salaam na wa vituo vya mpakani vya Tunduma, Mtukula, Holili na Kasumulo, wahamishiwe maeneo mengine.
 
Kundi jingine alilotaka lihamishwe ni watumishi wote waliokaa kwa zaidi ya miaka mitatu katika vituo hivyo.
 “Hatua hii inayochukuliwa sasa  ni mwanzo tu wa mabadiliko makubwa yatakayofanywa katika Idara ya Uhamiaji ili kuboresha huduma zinazotolewa na idara hii ambayo ni moja idara muhimu za serikali.”
CHANZO: NIPASHE


author

This post was written by: Author Name

Your description comes here!

Get Free Email Updates to your Inbox!

Post a Comment

CodeNirvana
© Copyright MAWINGUBONGO
Back To Top