Wakati vyombo vya uchunguzi vikiendelea kuchunguza tuhuma zinazowakabili baadhi ya wabunge kwa kupokea rushwa kwenye Kamati za Bunge, Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba, Maendeleo ya Makazi, Angelina Mabula, amesema Bunge linapaswa kujisafisha.
Mabula ambaye pia ni Mbunge wa Ilemela, alitoa kauli hiyo wakati akizungumza na Nipashe baada ya kumalizika kwa ibada ya mkesha wa Pasaka katika Kanisa la Mtakatifu Petro.
Alisema kama tuhuma za rushwa zinazoelekezwa katika Bunge zina ukweli, Bunge linapaswa kujisafisha kwa kuwa ni mojawapo wa mhimili wa serikali unaotumainiwa na wananchi.
Alisema Watanzania wana imani kubwa na wabunge katika kuwatatulia kero zao kwa kuwa wao ndiyo wawakilishi wa wananchi, hivyo tuhuma zinapowakabili wanapaswa kijisafisha na kuwa wasafi.
“Siwezi kuzungumza kwa undani zaidi kwa kuwa sote hatujui kama ni kweli au la, lakini ninachoweza kusema ni kama tuhuma hizo zina ukweli, basi Bunge linapaswa kujisafisha,” alisisitiza Mabula.
Kadhalika, amewaasa Watanzania kutenda matendo mema wakati wote.
Kumekuwapo na tuhuma za rushwa kwa baadhi ya wenyeviti wa Kamati za Bunge, huku wabunge wengine wakijiuzulu kwa kutaka mamlaka za kiuchunguzi wachunguze tuhuma hizo na sheria ichukue mkondo wake.
Baadhi ya wabunge wanaotuhumiwa kupokea rushwa ni wa Kamati ya Maendeleo na Huduma za Jamii, hali iliyosababisha wabunge 12 katika kamati hiyo kusaini waraka maalum wa kupelekwa kwa Spika kutaka kujiuzulu, huku Spika wa Bunge, Job Ndugai, akifanya mabadiliko ya wenyeviti watano wa kamati hizo.
CHANZO: NIPASHE
Post a Comment