MBUNGE wa Mtera mkoani Dodoma, Livingstone Lusinde (CCM), ameapa kutowaonea haya watumishi watakaobainika kuhusika na wizi wa dawa katika vituo vya kutolewa huduma jimboni mwake.Lusinde, maarufu kama Kibajaji, aliyasema hayo jana alipokuwa akizungumza na Nipashe, juu ya mikakati ya kuboresha huduma za afya, ikiwamo upatikanaji wa dawa katika zahanati na vituo vya afya katika jimbo hilo.
Alisema katika hatua za awali, atahakikisha kiasi cha dawa kinachopelekwa na Bohari Kuu ya Dawa (MSD) katika zahanati na vituo vya afya, kinaongezwa ili kukidhi mahitaji ya ongezeko la watu.
“Tutanza na kuongeza idadi ya dawa kwani hivi sasa hatuwezi kusema moja kwa moja kuwa kuna wezi kwani idadi ya watu imekuwa ikiongezeka kila kukicha, lakini kiasi cha dawa hakiongezeki, hivyo kusababisha watu wengi kukosa dawa,” alisema.
Alisema baada ya kuongeza kiwango cha dawa, kazi itakayofuata ni kusimamia utoaji na usambazaji ili kuangalia kama kuna wizi unafanyika au la.
Lusinde aliongeza kuwa kwa kushirikiana na Mganga Mkuu wa Wilaya (DMO), watasimamia vituo ambavyo vimekuwa vikitoa huduma chini ya kiwango, hivyo kusababisha watu kukimbilia zahanati ambazo zimekuwa na unafuu.
“Tutawasimamia watumishi ambao wamekuwa hawafanyi kazi zao kwa ufanisi na kusababisha foleni ndefu za wagonja katika zahanati moja kwa madai kuwa ndiyo inayotoa huduma nzuri zaidi ya zingine,” alisema.
Pia alisema atahakikisha watumishi ambao wamekuwa wakicheleweshewa mishahara yao wanapewa kwa wakati ili kuwaongezea ari katika kufanya kazi.
==>IPPMEDIA
Post a Comment