Chama cha mapinduzi (CCM) kimeibuka kidedea katika uchaguzi wa ubunge Jimbo la Ulanga baada ya mgombea wake, Goodluck Mlinga kupata kura 25,902 sawa na asilimia 69.78 akiwashinda wapinzani wake katika uchaguzi uliofanyika jana wilayani Ulanga mkoa wa Morogoro.
Akitangaza matokeo ya uchaguzi huo katika Ukumbi wa Halmashauri ya wilaya ya Ulanga usiku wa kuamkia leo, Isabela Chilumba alimtangaza mgombea wa CCM, Goodluck Mlinga kuwa ndiye mshindi wa kiti hicho baada ya kuwabwaga wenzake wa chama cha Demokrasi na Maendeleo (CHADEMA) na ACT-Wazalendo.
Mgombea wa CHADEMA Pancras Michael Ikongoli alipata kura 10,592 sawa na asilimia 28.53 wakati mgombea kupitia ACT-Wazalendo yeye akipata kura 6,26 sawa na asilimia 1.69
Uchaguzi huo umefanyika Novemba 22 ikijumuisha vituo vya kupigia kura 203 katika kata 21 huku kukiwa na idadi ya wapigakura 76,715 waliojiandikisha katika daftari la kudumu la wapigakura.
Jumla ya wapigakura 37,499 walijitokeza kupiga kura huku kura 379 zikiharibika wakati kura halali zikiwa 37,120.
Kwa upande wa mgombea wa CCM, Goodluck Mlinga aliwashukuru wananchi wa jimbo la Ulanga kwa kumchagua kuwa mbunge wao na kuahidi kuitumikia kazi hiyo kwa moyo mmoja na kuomba ushirikiano kutoka kada mbalimbali ili kutekeleza majukumu yake hayo mapya.
==>jamiiyetubongo.com
Post a Comment