HATIMAYE Charles Lugiko ambaye ni baba mdogo wa aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Mkoa wa Geita, marehemu Alphonce Mawazo, amefungua kesi ya kupinga uamuzi wa Jeshi la Polisi, Mkoa wa Mwanza, kuwazuia kuaga mwili wa mtoto wao.
Kesi hiyo ilifunguliwa jana katika Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza ambapo wanasheria watatu wa Chadema walijitokeza kwa ajili ya kumtetea.
Jeshi hilo, lilizuia mwili wa marehemu Mawazo usiagwe jijini Mwanza kwa kile walichoeleza, kwamba kuna ugonjwa wa kipinduipindu na kuwataka ndugu na viongozi wa Chadema, kuuchukua katika Hospitali ya Rufaa Bugando na kwenda kuuaga mkoani Geita ambako ni nyumbani kwa marehemu.
Akizungumza na waandishi wa habari nje ya Mahakama Kuu, Kanda ya Mwanza, Mwanasherisa wa Chadema, John Malya, alisema wameamua kufungua kesi ya madai namba 10 ya mwaka 2015, kuitaka mahakama kuondoa zuio la Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Charles Mkumbo, kuzuia mwili wa marehemu Mawazo usiagwe.
Malya alisema kesi hiyo ya dharura, imefunguliwa na baba mdogo wa marehemu Mawazo, Lugiko, akitaka mahakama kutengua zuio la polisi la kuaga mwili wa ndugu yao jijini Mwanza.
“Kesi imesikilizwa upande mmoja wa mlalamikaji, sasa kwa bahati nzuri Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza, Lameck Mlacha, ametueleza kwamba kutokana na umuhimu wa kesi hii, ataiendesha kwa uharaka wake, kesho (leo) itaendelea kusikilizwa baada ya kupewa nyaraka za kesi husika.
“Kuna kitu kimetokea hapa hapa na watu wanahoji kwanini kesi imesikilizwa katika Jengo la Mahakamu Kuu, Kitengo cha Biashara, hilo sisi hatujali, maana popote jaji anapokaa ni mahakama,” alisema Milya.
Naye mwanasheria mwingine katika kesi hiyo, James Milya, alisema anashangazwa na Jeshi la Polisi kuwazuia wananchi kuingia katika viwanja vya mahakama pamoja na kuweka ulinzi mkali katika ofisi za Chadema, huku akiahidi kuhoji suala hilo mahakamani wakati kesi hiyo ikisikilizwa.
WANANCHI WAFURIKA MAHAKAMANI
Wakati hayo yakiendelea, wananchi walifurika katika Mahakama Kuu, Kanda ya Mwanza, kusikiliza kesi hiyo licha ya polisi kutanda kila kona wakiwa na silaha mbalimbali za moto pamoja na mabomu ya machozi kujaribu kuwazuia.
Pamoja na zuio hilo, wananchi walitumia mbinu ya kuingia mahakamani hapo mmoja mmoja na hatimaye kujikuta wakijaa mahakamani hapo bila kutarajia.
Baada ya askari polisi kuona watu wameshajaa, walishindwa kuchukua hatua dhidi yao na hivyo kuwaacha waendelee kuwapo mahakamani hapo.
Wananchi hao walianza kuwasili katika viwanja vya mahakama saa mbili asubuhi hadi kesi hiyo ilipoanza kusikilizwa saa nane mchana.
MBOWE AWASILI
Wakati kesi hiyo ikisubiri kusikilizwa, ilipotimia saa 7.25 mchana, Mwenyakiti wa Chadema, Freeman Mbowe, aliwasili katika viwanja vya Mahakama Kuu akiwa katika ulinzi mkali na kusababisha wananchi waliokuwa mahakamani hapo kumzingira huku kila mmoja akitaka kumsalimia.
Kutokana na hali hiyo, Mbowe aliwataka wananchi kuwa wapole kwa kuwa eneo hilo halihitaji kelele au ishara zozote za vyama vya siasa, kisha aliingia mahakamani na kukaa kwa dakika 15 kabla hajatoka nje na kuelekea katika jengo ambalo kesi hiyo ilisikilizwa.
Wakati mwanasiasa huyo akitembea kwa miguu kuelekea katika ukumbi ilikokuwa ikisikilizwa kesi hiyo, kundi la wananchi waliokuwa mahakamani hapo lilimfuata na kusababisha kufungwa kwa barabara ya Posta huku magari yakishindwa kupita.
Kutokana na wingi wa watu, askari polisi waliokuwa mahakamani hapo, walishindwa kuwadhibiti na badala yake waliamua kuwasindikiza katika hali ya utulivu.
Wakati akizungumza na wananchi hao, Mbowe alisema jaji anayesikiliza shauri hilo, alikuwa amesikiliza upande wa mlalamikaji, na kwamba leo upande wa walalamikiwa ambao ni Jeshi la Polisi na watasikilizwa.
==>habarikali1.com
==>habarikali1.com
Post a Comment