Mbunge wa Jimbo la Ubungo Saed Kubenea, ametembelea Hospitali ya Palestina iliyopo Sinza jimboni humo, ili kujionea utendaji wa kazi na mahitaji ya wagonjwa.
Katika ziara hiyo, Kubenea alishtushwa kukuta hospitali hiyo ikiwa na vitanda vichache katika wodi ya wazazi, huku za wakina mama waliojifungua kwa upasuaji, waliojifungua kawaida na wanaosubiri kujifungua zote zikiwa na vitanda 11 tu.
Changamoto nyingine aliyoktana nayo ni ufinyu wa eneo la hospitali, uhaba wa majengo, vitendea kazi na ubovu wa miundombinu.
Akizungumza akiwa hospitalini hapo, Kubenea alisema serikali inapaswa kuongeza nguvu na kupeleka samani za kutosha pamoja na vifaa tiba hasa ikizingatiwa idadi ya watu wanaofika na kupata huduma hospitalini hapo inaongezekana kila siku.
"Baada ya kuona hali hiyo, jukumu langu la kwanza ni kutafuta fedha kutoka kwa wafadhili ili wasaidie upatikanaji wa vifaa tiba kwa lengo la kuboresha huduma na mwisho wa siku hospitali ilingane na hadhi ya wilaya iliyonayo," alisema Kubenea.
Pia alisema atahakikisha kupitia fedha zitolewazo na serikali katika hospitali hiyo zinatumika vizuri ili kubadilisha muonekana wa hospitali na kutatua changamoto zilizopo.
Kwa upande wake, Kaimu Mganga Mfawidhi wa hospitali hiyo, Dk.Hugolin Mselle, alisema moja kati ya mikakati iliyopo ni kuhakikisha nusu ya pato linalotokana na uchangia gharama za matibabu kwa wagonjwa linabaki ndani ili litumike kuboresha huduma za akina mama wajawazito.
"Kutokana na ugumu wa maisha kwa baadhi ya wanachi, hospitali imeamua nusu ya pato linalokusanywa litumike kuhudumia akina mama hao kwani tutaokoa kizazi kijacho," alisema.
Dk. Mselle alisema uhaba wa vitanda na uhaba wa majengo unasababisha akina mama waliojifungua kutokaa wodini kwa muda unaostahili ili kupisha wengine wapate huduma hiyo.
Alisema kwa sasa hospitali inapokea wajawazito 20 hadi 60 kwa vipindi tofauti na wote wanahitaji huduma ya vitanda hivyo vichache.
Kubenea pia alitembelea ofisi za Manispaa ya Kinondoni ambako alikutana na Mhandisi Mkuu wa Majengo, Baraka Mkuya na kushauri uwekwe utaratibu wa kutoa taarifa za kuwapo kwa ubomoaji wa nyumba ili kuwapa wananchi nafasi ya kufanya maandalizi.
==>ippmedia
Post a Comment