Makocha wawili wa zamani Yanga, Milutin Sredojovic 'Micho' na Tom Saintfiet, mwishoni mwa wiki iliyopita walitambiana wakati timu za taifa wanazofundisha kukutana katika mchezo wa marudiano kuwania nafasi ya awali kufuzu Kombe la Dunia mwaka 2018 nchini Russia.
Micho, raia wa Serbia anayefundisha Timu ya Taifa Uganda (The Cranes), aliibuka na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Togo inayofundishwa na Saintfiet, raia wa Ubelgiji.
Kwa ushindi huo, Uganda imefuzu hatua ya makundi kwa jumla ya mabao 4-0 baada ya mchezo wa kwanza ugenini kushinda 1-0, kisha 3-0 kwenye mechi ya marudiano iliyochezwa Kampala, Uganda.
Kocha Micho alimuanzisha beki wa Simba, Murshid Juuko, huku Hamisi Kiiza aliyeonyeshwa kadi ya njano mchezo wa kwanza, akikaa benchi kama ilivyokuwa kwa mwenzake, beki Yanga, Vincent Bossuo, ambaye yeye hakucheza ugenini wala nyumbani.
Katika hatua nyingine wachezaji Amissi Tambwe wa Yanga baada ya kukaa benchi katika mechi ya kwanza wakati Burundi ilipoikaribisha Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), juzi wakiwa ugenini, aliingia uwanjani zikiwa zimebaki dakika 28, wakati Didier Kavumbagu wa Azam FC alicheza dakika 10 za mwisho katika mechi ya sare ya 2-2.
Kongo walisonga mbele katika michuano hiyo kwa kuifunga Burundi jumla ya magoli 5-4, huku mshambuliaji anayewania na Simba, Laudit Mavugo akisugua benchi kwa dakika 180.
Baadhi ya matokeo ya mechi nyingine za michuano hiyo mwishoni mwa wiki, Zambia walisonga mbele kwa ushindi wa mabao 2-0, wakishinda bao 1-0, nyumbani na ugenini.
Equatorial Guinea yenyewe ilishinda bao 1-0 dhidi ya Morocco, wakati Guinea iliilaza Namibia mabao 2-0.
Kwaa ukanda wa Afrika Mashariki na Kati, Kenya iliyopata ushindi wa bao 1-0 katika mechi ya kwanza Ijumaa jijini Nairobi, itashuka leo ugenini kurejena na wenyeji wao Cape Verde, wakati Rwanda iliyolala kwa bao 1-0 watakuwa nyumbani kuwasubiri Libya.
IPPMEDIA
Post a Comment