Wakati makundi mbalimbali ya kijamii yakiungana na Rais Dk. John Magufuli kufanya usafi katika maeneo mbalimbali nchini, Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), hawajashiriki tukio hilo kwa misingi ya chama.
Ukawa ambao unaundwa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), NCCR-Mageuzi, NLD na Chama cha Wananchi (CUF), haukushiriki tukio hilo kwa ulichoeleza halikuwa la vyama bali la Watanzania wote.
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Chadema, Tumaini Makene, jana alilieleza Nipashe kuwa, tukio hilo la usafi nchi nzima halikuwa likihusisha vyama, hivyo Ukawa haukuona sababu ya kushiriki. “Kama ni usafi Rais ameagiza wananchi wote washiriki kikamilifu na siyo suala la chama ndio maana Ukawa hatujashiriki bali tumeshiriki kama wananchi wa kawaida ikizingatiwa kuwa siku ya usafi siyo lazima iwe moja bali usafi ni kila siku,” alisema Makene.
Aidha, Makene alisema viongozi wa Chadema wako mkoani Arusha kwa ajili ya kampeni za mgombea ubunge wa jimbo hilo, Godbless Lema.
“Kwanza viongozi wa Chadema wakiongozwa na mwenyekiti wetu, Freeman Mbowe, wako mkoani Arusha wanafanya kampeni kwa ajili ya uchaguzi utakaofanyika Jumapili,” alisema.
Wakati Makene akisema hayo kuhusu Ukawa, Mbunge wa Kigoma Mjini kupitia Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe, alishirikiana na wananchi wa jimbo lake kufanya usafi katika Zahanati ya Rusimbi iliyopo kata ya Rusimbi.
CHANZO: NIPASHE
Post a Comment