Mwanamuziki anayekimbiza Afrika na kwingineko duniani, Nassib Abdul almaarufu kama Diamond Platnumz, amemwaga mchele hadharani na kumtaja zilipendwa wake Wema Sepetu kuwa ana mambo ya Kiswahili. Diamond aliyasema hayo jijini Dar es Salaam hivi karibuni akijibu mapigo kufuatia kauli za kejeli aambazo Wema alizitoa dhidi yake.
![]() |
Diamond Platnumz na Wema Sepetu enzi za uwili wao |
Awali "Beautiful Onyinye" Wema Sepetu alimshushia mipasho Diamond Platnumz kwamba alimnunulia zawadi ya gari la bei chee, akisema kuwa liligharimu shilingi za Tanzania elfu thelathini. Wema alimwaga upupu huo Jumapili ya tarehe 1 Novemba katika “birthday party” yake aliyoifanya hivi karibuni katika ukumbi mmoja uliopo katika jengo la Millennium Towers jijini Dar es Salaam. Mnyange huyo alitumia nafasi hiyo kuwaonesha wageni waalikwa gari alilojinunulia mwenyewe na kujizawadia. Alisema kuwa gari hilo aina ya Range Rover limemgharimu dola za Marekani 90,000 ambazo ni sawa na zaidi ya shilingi milioni 190 za Tanzania.
![]() |
Diamond Platnumz |
Akiongea kwa utulivu mkubwa, Diamond Platnumz alimpongeza Wema kwa kununua gari kwa kuwa hiyo ndiyo ilikuwa mipango yake. Hata hivyo mkali huyo wa Afro Pop alisema hatua aliyofikia yeye si ya kushindana kununua magari tena, na kudai kuwa hatua hiyo yeye ameshapita. Diamond alisema katika maisha kila mmoja ana ndoto zake. Alisema kuwa yeye amefanikisha ndoto zake na katika hatua aliyofikia hana sababu ya kufanya mashindano na mtu, badala yake anahitaji kujituma zaidi ili kusaka mafanikio makubwa zaidi.
“Hayo ndiyo mambo ya Kiswahili,” alisema Diamond Platnumz ambaye siku za karibuni amekuwa akijulikana pia kama ‘Baba Tiffah’. "Najua kuna watu bado wanafikiri mimi ni limbukeni wa vitu kama zamani. Kwa sasa sifikirii mashindano, naangalia kazi zinazoweza kuniingizia kipato tu,” alisema Diamond Platnumz.
Post a Comment